|
TAANASI NA MAPOKEZI YA KALE YA WA-MVITA Na Ahmed Hussein Ahmed, B.A. , M.A., Dip. Ar.
TAQADIMU
Mapokezi ya kale ya wa-mvita’ yaliweza kuchukua sehemu moja ya Fasihi simulizi ambayo ilitumbuiza, nasihi, taanasi, sherehesha, kutoa taazia na kwa malengo mengineyo. Maarufu zaidi katika mapokezi hayo ni matumbuizo ya watoto wakati wa faragha (mapumziko) na wanapojianda kwenda kulala Wazee wa kale wa Kiswahili walikuwa na namna nyingi za kuwatumbuiza watoto wao. Kati ya namna hizo ni kuwaimbia vipokeo, kuwatolea hadithi, mashairi na nyimbo mbali mbali nyakati za jioni Wakati mwengine watoto na vijana wa marika mamoja wanapopata nyakati za faragha hujitumbuiza kwa vipokeo na michezo kadha wa kadha Makala haya yatahusisha baadhi ya mapokezi hayo 2. Mkazo zaidi utatiwa katika mapokezi ya watoto na vijana wa kimvita Msomaji apaswa kufahamu kuwa mapokezi kama haya huweza pia kupatikana katika sehemu nyengine za Afrika mashariki na pengine janibu ya sehemu hizo.
UKALE WA MAPOKEZI Bado hakujajulikana ukale hasa wa mapokezi haya. Kulinganana baadhi ya mapokezi yanatufanya tutoe makisio fulani juu ya tarehe ya mapokezi hayo. Kwa mfano “Peepepepeta Wazungu wawili wapitaWan ‘kovu za kitwa Wakitoneshana wateta Sara n’tokapi na ulingo ‘toka n'komani Baulingo..." Mapokezi haya yanakisika kuwepo tokea karne ya kumi na tano ambapo wareno na wazungu wengineo walikuwa wameshawasili sehemu za Mvita. Halikadhalika, kutajwa kwa neno "shilingi" inatueleza kuwepo kwa matumizi ya sarafu katika kame kumi na nane au pengine kabla yake. Mfano wa mapokezi yenye kutumia neno hilo Ia sarafu tulilo nukuu hapo juu ni huu ufwatao: "Shilingi yangara yaua (kipokezi hurudiwa mara mbili), sijauona mpili pili na maua yake mchikichoo...." Yaamkinika pia ,baadhi ya mapokezi haya ni ya jadi najadi Katika baaadhi ya sababu zinazotufanya tudhanie hivyo ni kule kuwepo kwa istilahi za kale na/au zilizo sahaulika3. MAUDHUI NA MALENGO YA MAPOKEZIMapokezi ya watu wa kale yalikuwa na malengo na maudhui mbalimbali. Yapo yaliyodhamiriwa kutumbuiza, kufunza vijana, kuwashajiisha,na kuwaongoza wawe ni watoto wema wenye nidhamu. Mapokezi haya yalitumika nyakati za kupasha jando, harusi, mavuno na wakati wa huzuni na misukosuko. ‘Kisiwa cha Mvita sasa chafahamika zaidi kwa jina Ia ‘Mombasa’ Hapa ndipo mahali mwandishi alipozaliwa na alipokulia. Maandishi mengi ya kale yametumia neno ‘Mvita’ kuliko jina lenginelo. Hii ni moja ya sababa muandishi amependelea kutumia jina hilo katika makala haya. Natoashukurani nyingi kwa dadaangu Bi. Leyla Ali Abdalla (b. 1962) wa Magongo, Mombasa, ambaye alitumia wakati wake mrefu kunisimuliya na kunitolea kimahadhi baadbi ya mapokezi haya, 10 Desemba, 1998.. 3 Mahojiano yangu na mzee wangu Shelkh Ahmad Nabahany, mtafiti mashuhuri wa lugha ya Kiswahili, Mombasa, Swahili Cultural Centre 21 May,1998. MAPOKEZI YA WATOTO NA MICHEZO YAO Watoto na vijana hujumuika pamoja kwa matumbuizo na taanasi mbali mbali hususan nyakati za jioni Mara nyengine katika sherehe rasmi, wakunga na wavyele hukusanyika kuwaongoza vijana hasa wanaobaleghe na wanaokaribia kufunga ndoa Michezo marufu ya watoto wa Kiswahili tangu zama hizo ni pamoja na kucheza kibe ndolee, ulimbo, tega n'kutege, blada, nusu mkalili, kuruka kamba, Kurusha tiara,mieleka, kirumbizi, kupiga goma (ya ropa), na michezo mengineyo. Nyakati nyigine wavyele wanapopata faragha huwatumbuiza watoto wao kwa qasida, mashairi, haditbi, vitendawili na mapokezi mbali mbali. Yafuatayo m baadhi ya mapokezi hayo: Bibi songa nyele Bibi songa nyele shanuo la nini? Kitwa chaniuma dawa yake nini? Ponda tangawizi upake nyusini, Mahaba sindano ya choma maini
Aliyomi Al yomi aliyomi alimsabaha ilyomi, Kuna mnazi mmoja wapanda watu watatu Akianguka mmoja, Hamadi mwana wa watu. Ndege ruka ndege ruka na barua mdomoni Ukufika ukafika mbwagie mapajani. Usinione nimekonda ukadhani kwetu sili Nala mtele kibaba na nyama nusu ratili Kitoria baa kitoria baa Kahela kahela kajumbaka. Pepeta Peepepepeta Wazungu wawili wapita Wan ‘kovu za kitwa Wakitoneshana wateta Sara n n'tokapi na ulingo Natoka mkomani kunwa tembo Kesho n'tashuka Marekebu Na zinga lamoto Ia dhahabu. Sukuma kidau tunende Kwa Bwana Hamadi Madende Tukampokonye maembe Na wali mtamu kwa tende Mariamu na mpishi wake (Kipokezi hiki hurudiwa mara mbili). Ukuti wa mnazi Ukuti ukuti Wa mnazi wa mnazi Ukingia upepo Wan ‘tetema Wan ‘tetema Msegeju Msegeju ana ngombe Nami n ‘no ngombe zangu Namwambia tutanganye Hataki Kwa heri nenda zangu. Mapokezi ya Harusini Bibi harusi ndoo kaole Kaole mgeni kangia Mgeni kongo Aya eei Mgeni kangia. Hongera mwanangu ee Hongera nami nihongere mwana eei Mama uchungu mwana uchungu Eei Nyamala mwonangu siliye oyee Tumbo la uvyere linaumo mno eei Linauma mno hoyee!
Sema yuwapi mamake harusi aje hapa Tuhangaike naye (kipokezi) Na ndugu yake harusi aje hapa Tuhangaike naye Na rafiki yake harusi aje hapa tuhangaike naye... Aje amfunze mwari Asije kufedheheka Amwitikie mumewe kwa kila anachotaka.. 4
Mapokezi yanayotolewa na tanaasiYapo mapokezi ambayo watoto wa mvita huyatowa huka wakitaanasi u kucheza michezo mbali mbali. Baadhi ya taanasi hizo m michezo mbaiimbaii nayo huchezwa hivi: 4Rajiisha maelezo ya nambari 2 (mbili) hapo juu. Ulimbo Katika ulimbo wasichana hufanya mviringo wakishikana mikono. Binti yeyote hutajwa na kuingia kati kati ya boma akicheza kwa maringo huku akiimbiwa Ulimbo bayoyo baa Binti fulani piga goti tukuoneBingili bingili mpaka pwani Barua kwa baba Kijana hushika barua au mfano wake na kuzunguka nje ya boma Ia waliokaa chini huku akiimba “Napeleka barua kwa baba”. Kijana huyo atazunguka huku akilenga mtu wake kimoyomoyo. Anapomkaribia atamgusa na huku akitimka mbio. Aliyeguswa naye atamfurusha huyo mwenye barua hadi amshike. Akishindwa kumshika mwenye barua basi alochukua yeye barua na kufanya kama mwenye barua wa kwanza alivyofanya. Mwenye barua huimba mapokezi yake hivi:
Napeleka barua kwa baba, ikanipotea ndiani(Hurudiwa mara mbili) Si wewe, na si wewe, ni wewe... (mwenye barua akifanya uchaguzi wake). Kipara ngoto Anaye nyoa nyele (kipara) hugolewa na wenzake na kuimbiwa:
Kipara ngoto, maji yamoto Ukimpata mtie ngoto.
KidengeleAnaye onaekana na kitu chepesi kama vile sufi au unyoa utosini mwake pasi na yeye mwenyewe kujitambua, hugolewa na wenzake na kuuimbiwa: Mtu wangu an ‘kidengele Kesho ‘tam nyoa nyele.
Matezo ya simba Katika mchezo huu mmoja wa wanadi katika vijana atajifinya ni baba anaye nadi kuwatahadharisha watoto wake juu ya udhalimu na uvamizi wa simba. Mnadi huyo kumbe nimvamizi pia. Hivyo basi atanadi na wenziwe kumuitikia mnadi anapofika pale kwenye msemo usemao ‘nashuka chini ‘mnadi ataruka na kuwatimua mbio vijana wenziwe hadi amshike mmoja wao. Mapokezi ya ‘matezo ya simba’ ni haya yafuatayo: Mnadi: Watoto wangu eeh! Wapokezi: Eeeh! Mnadi: Mimi baba yenu Wapokezi: Eeeh! Mnadi:Sina nguvu tena eee ya kuua simba. Wapokezi: Eeeh! Mnadi:Simba m mkali eeh! Wapokezi: Eeeh! Mnadi:Aliua mama eels!, akaua nyanya eels!, akaua ndugu eels! akaua... Wapokezi: Eeeh! Mnadi: Nani kamata? Wapokezi’Mimi kamata, kama mume kweli kama mke kweli sishuka chini Mnadi: Haya nashuka chini(Mnadi ataruka na kuanza kuwatimuwa mbio wenzake hadi amshike mmoja wao). Kizuizui Mchezaji hufungwa macho (kizui zui) zw) kwa lengo Ia kushika mtu katika kundi la wachezaji wenziwe. Anaye shikwa naye atafunga kizuizui 5. Mpunga na nyama na uliwe Mpunga na nyama na uliwe ni mchezo ambao vijana hukusanya mlima wa mchanga na kijiti Kikawe kwa juu yake. Wachezaji huwa wawili au watatu. Kila mmoja huvuta mchanga polepole upande wake kwa vidole vya mikono miwili hadi kijiti kianguke upande wa mshindi Haliya totore Wale wanaoshindwa katika michezo mwisho huimbiwa Waliyataka wenyewe, haliya totore. ilobaki n ‘shauri yao NgomaZifuatazo ni baadhi ya ama ya ngoma maarufu zilizokuwa zikipigwa kisiwani Mvita hadi kufikia wakati wa uhuru 1963 Ngoma hizo za kale zilizosifika ni Kirumbizi, Twari la Ndia, Vugo7 Lele mama, Chakacha Mdodoki, sengenya Kimanyema Mabumbumbu, Namba, Gwaride, Twarabu, Sumsumiya, Mwaribe, Sindimba, na Mwanzele. Ngoma chache mno bado zingaliko kisiwani Mombasa pindi makala haya yalipotayarishwa na mwandishi. Baadhi ya ngoma tulizonukuu hapo juu zimekufa baada kukemewa na kupingwa na mashekhe na wanazuoni Afrika Mshariki TAKHATIMU Makala haya yamejaribu kwa kiasi fulani kutoa maelezo juu ya mapokezi na taanasi mbali mbali za wa-Mvita. Mapokezi haya ambayo yanakaribia kutoweka na mengine kusahaulika kabisa yaliweza kutumbuiza, kuongoza, kufunza, kushajiisba, kufurahisha na kuhuzunisha hadhirina mbalimbali. Mapokezi haya yaliweza pia kujenga maadili, dasturi na adabu za watoto wa Kiswahili. Fasihi simulizi kama hii iliongeza ladha utamu wa lugha na kukipamba Kiswahili Hapo ndipo tukasema ‘kila msimu ukija huja na yake’ Haki za kunakili ni za c- Ahmed Hussein Ahmed 5 Mahojiano yangu na Sheikh Mohammad AbdulRahman (b. 1940), Mombasa, 28th May 1998. Halikadhalika, natoa shukurani kwake na kwa wengine ambao sikuwataja hapa kwa usaidizi wao walionipa katika kukusanya na kuziandika baadhi ya mapokezi na taanasi za wa-Mvita. 6 Rajiisha namba 5 (tano) hapo juu. 7 Ngoma ya ‘vugo’ bado ingali maarufu upande wa Lamu na Siyu
|